Wakati tume ya kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012 ikiendelea na kazi, imebainika kuwa wanafunzi waliokata rufaa kutaka mitihani yao isahihishwe upya wamefeli zaidi baada ya kusahihishiwa.Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambazo zimethibitishwa na baadhi ya maofisa, wanafunzi waliokata rufaa wamefeli zaidi na hata walioongezewa alama matokeo hayakubadilisha madaraja waliyopata awali.Habari zinaeleza kuwa, wanafunzi waliokata rufaa NECTA kutaka mitihani yao isahihishwe upya ni takribani 10,000 na kwamba baraza bado limetoa muda zaidi kwa wengine wanaotaka kukata rufaa. Vyanzo vya habari kutoka ndani ya NECTA viliieleza NIPASHE kuwa mitihani kwa wanafunzi waliokata rufaa ilianza kusahihishwa Machi 12 na kuhitimishwa Machi 15, mwaka huu na kwamba wengi wamefeli zaidi.“Baada ya wanafunzi kadhaa kukata rufaa, NECTA iliamua kuwaita walimu waandamizi katika masomo yote na kuanza kufanya kazi ya kusahihisha mitihani hiyo upya kwa umakini, kilichowashangaza walimu hao ni kuona kiwango cha kufeli kimeongezeka,” alisema ofisa mmoja wa NECTA ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa maelezo kuwa siyo msemaji wa baraza hilo.
Baadhi ya walimu walisema walioshiriki kusahihisha mitihani hiyo walisema kuwa maoni yaliyokuwa yanatolewa na baadhi ya watu kwamba matokeo mabaya ya mtihani huo yalitokana na uchakachuaji, hayakuwa ya kweli.Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Ndalichako, akizungumza na NIPASHE jana alithibitisha kuwa mitihani ya wanafunzi waliokata rufaa ilianza kusahihishwa Machi 12 mwaka huu.
Dk Ndalichako alisema hata hivyo, hana taarifa kama matokeo ya wanafunzi hao yanaonyesha kuwa wanafunzi wengi wamefeli zaidi kwa kuwa alikuwa safarini kikazi.“Unavyozungumza na mimi nipo Arusha na wageni, sifahamu kama baada ya kusahihishwa upya mtihani wa wanafunzi waliokata rufaa matokeo yamekuwaje, nitafahamu baada ya kurejea Dar es Salaam Jumatano wiki hii,” alisema Dk Ndalichako ambaye hata hivyo, hakutaja idadi ya wanafunzi waliokata rufani.Dk Ndalichako alisema suala la kufeli zaidi wanafunzi waliokata rufaa linawezekana kutokea kwa sababu kila mwaka imekuwa ikijitokeza hali kama hiyo, hivyo ni jambo la kawaida.
Habari kwa Hisani ya Wizara ya Elimu Tanzania... |
No comments :