Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, Moses Malaki alisema jana kwamba ratiba za uwanjani
hapo zitabadilika kutokana na uzito wa ugeni huo.
Alisema kwa kawaida anapokuja kiongozi mkubwa wa
kitaifa katika uwanja huo hakuna ndege inayoruhusiwa kutua kwa kipindi cha nusu saa.
“Ni kweli hali hiyo pia itakuwapo
atakapokuja Rais Obama na safari
za ndege zitabadilika kulingana na ratiba ya kutua na kuondoka kwa
Rais huyo,” alisema Malaki.
Pia alisema ulinzi katika uwanja huo umeimarishwa
kwa mwezi mmoja sasa na tangu wakati huo,
maofisa wa usalama wa Marekani wamekuwa wakifika kwa nyakati mbalimbali.
“Sijawahi kuona ulinzi mkali kama huu, wamekuja
marais wengi hapa nchini lakini ulinzi huu ni wa kutisha, sijui
kwa sababu gani?” alisema Malaki.
Alisema awali, wakati maofisa hao walipoanza
kuwasili nchini hawakutambua ni mgeni
gani anayetarajia kufika lakini baadaye walipelekewa taarifa kuwa ni Rais
Obama na baadaye walitaarifiwa kuwa angetua saa 8.40 mchana, Julai Mosi.
Mkurugenzi huyo alisema Rais Obama atakuja
na ndege nne, moja itakayombeba,
ya pili kwa ajili ya mizigo, ya tatu itakuwa ya waandishi
wa habari na maofisa wa usalama na ya mwisho ni kwa ajili ya dharura ambayo itaegeshwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA)
Malaki alisema maofisa wa Marekani wanaowasili nchini wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kuhakikisha kuwa hali ya usalama
inaimarishwa na kuwaacha wazawa wakifanya shughuli za kawaida.
“Ulinzi ni mkali mno, yapo masharti kadhaa
wanayoyataja kuwa yatatumika
kwa watu watakaoingia
eneo la uwanja au kuisogelea ndege ya Rais Obama. Jamaa
wameweka masharti magumu,” alisema.
No comments :